Mshambuliaji Amis Tambwe ameitibua sherehe ya utambulisho wa
Emmanuel Okwi baada ya kupachika mabao mawili wakati Simba
ilipoichakaza Yanga 3-1 katika mchezo wa ‘Nani Mtani Jembe’ jana kwenye
Uwanja Taifa, Dar es Salaam.
Mrundi Tambwe alifunga mabao mawili huku Awadh
Juma akifunga bao moja kwa Simba kabla ya Okwi kufunga bao la kufutia
machozi kwa Yanga.
Tambwe aliwainua mashabiki wa Simba dakika ya 13
baada ya kupokea pasi nzuri ya Said Ndemla akiwa peke yake na kupiga
shuti pembeni kwa kipa Juma Kaseja.
Baada ya Simba kupata bao mashabiki wa Yanga
walikaa kimya hali iliyomfanya mwenyekiti wao Yusuf Manji kusimama na
kuwataka washangilie huku akionyesha vidole vitano. Jambo lililowafanya
mashabiki wa Simba kuanza kuzomea kwa nguvu.
Tambwe alipatia Simba bao la pili kwa mkwaju wa
penalti dakika ya 43 baada ya Ramadhani Singano kuchezewa vibaya na
David Luhende, kabla ya kuhitimisha kwa bao la tatu dakika ya 60,
akitumia vizuri uzembe wa Kaseja kupachika bao la tatu.
Manji aliinuka kwenye kiti chake na kwenda
kumkumbatia Zaccaria Hanspope na kuondoka uwanjani hali iliyowafanya
mashabiki wa Simba kumzomea.
Okwi aliingia akitokea benchi na kuifungia Yanga
bao la kufutia machozi dakika ya 79, akimalizia vizuri krosi ya Haruna
Niyonzima.
Mashabiki wa Simba walikuwa wakiwakejeli wenzao wa
Yanga kwa kuwaambia waendelee kusajili wachezaji wa Simba faida yake
wameiona.
Baada ya kukabidhiwa kombe mashabiki wa Simba
walizunguka nalo, na wengine wakisukuma gari la Hanspope huku wakiimba
‘Okwi, Okwi, Okwi..’
Katika mchezo huo Yanga walionekana kuwa na presha na kucheza zaidi kibinafsi kuliko kitimu kulinganisha na wapinzani wao Simba.
Yanga waliondoka kabisa mchezoni baada ya bao la
Simba na kuwaacha viungo Mkude, Henry Joseph, Chombo wakifanya watakalo
katika kuanzisha mashambulizi ya vijana hao wa Msimbazi.
Post a Comment