Maelekezo yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za
Serikali (PAC), Zitto Kabwe kutaka kusitishwa kwa ruzuku kwa vyama vya
siasa nchini kutokana na kutowasilisha taarifa za ukaguzi wa matumizi
yake, yamevivuruga baadhi ya vyama vilivyotajwa.Vyama vya siasa vinaonekana kutoa matamshi
yanayolenga kujinasua katika hoja hiyo, vikiwemo vilivyomshutumu Zitto,
kuilaumu Serikali na hata vingine vimediriki kutaka ruzuku hiyo ifutwe
kwa maelezo kwamba ni ubadhilifu wa fedha za umma.
Juzi Zitto alisema tangu 2009 Serikali ilitoa
kiasi cha Sh67.7 bilioni kama ruzuku kwa vyama tisa vya siasa, lakini
vyama hivyo havijawahi kuwasilisha taarifa za ukaguzi hesabu zake
msajili kama sheria inavyoagiza. Kwa sababu hiyo, Zitto aliamuru Ofisi
ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, kusimamisha utoaji wa ruzuku hadi
hapo vitakapowasilisha ripoti ya ukaguzi na makatibu wake wakuu
kuhojiwa.
Kwa mujibu wa Sheria namba 5 ya 1992 ambayo
ilifanyiwa marekebisho ya Sheria namba 7 ya 2009, Vyama vya Siasa
vinawajibika kuwasilisha hesabu zake kwa CAG na ofisi hiyo inaweza
kuamua kuzifanyia ukaguzi yenyewe au kuteua mkaguzi.
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG), Ludovick Utouh aliwahi kusema kuwa utaratibu ambao umekuwa
ukitumiwa na vyama hivyo kwa kuteua kampuni binafsi siyo sahihi na ni
kinyume cha sheria.“Kwa mujibu wa kifungu cha 14 cha Sheria ya Vyama
vya Siasa, vyama vinatakiwa viwasilishe hesabu kwa CAG, ndipo tuzikague
au tuamue kampuni ya kufanya ukaguzi huo, sasa wao walichagua kampuni
binafsi moja kwa moja zikawafanyia ukaguzi,” alisema Utouh wakati
akitangaza kuthibitisha ubora wa hesabu za vyama vitano vilivyoshiriki
kwenye Uchaguzu Mkuu wa 2010.
Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji
Christopher Mtikila alipendekeza kufutwa kwa ruzuku hiyo kwa vyama vya
maelezo kuwa ni inawanyonya wananchi.“Badala ya kuvipa vyama vya siasa ruzuku,
tuelekeze fedha hizo kwenye miradi mingine ya maendeleo,” alisema
Mtikila huku akiahidi kwamba chama hicho kitawasilisha kwa Msajili wa
Vyama vya Siasa taarifa yake ya fedha iliyokaguliwa katika kipindi cha
wiki mbili kuanzia sasa.
chanzo: http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Zitto-avitikisa-vyama/-/1597296/2035700/-/ewbfygz/-/index.html
chanzo: http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Zitto-avitikisa-vyama/-/1597296/2035700/-/ewbfygz/-/index.html
Post a Comment