Mshikamano wa vyama vya upinzani katika kupinga Muswada wa
Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa 2013 umehamia nje ya
Bunge na sasa vyama hivyo vimetangaza kuanza kampeni ya kuuhamasisha
umma kudai maridhiano kabla ya kuendelea na mchakato wa Katiba Mpya.
Jana wenyeviti wa vyama hivyo; James Mbatia
(NCCR-Mageuzi), Freeman Mbowe (Chadema) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF)
walikutana na waandishi wa habari na kumtaka Rais Jakaya Kikwete
kutosaini muswada huo kuwa sheria, hadi pale kutakapokuwa na maridhiano
ya pande zote husika.
Walisema muungano wao ni mwanzo wa kuunganisha
umma wa Watanzania kufanya uamuzi wa kunusuru walichokiita “utekaji
madaraka na mamlaka ya nchi kutoka kwa wananchi” hivyo wanaitaka
Serikali kurekebisha kasoro zinazojitokeza katika mchakato huo.
Akitoa tamko la pamoja kwa niaba ya viongozi
wenzake, Profesa Lipumba alisema wanachopigania ni kuurejesha mchakato
wa Katiba Mpya mikononi mwa umma, kwa maelezo kwamba suala hilo kwa sasa
limehodhiwa na CCM.
“Rais Kikwete asisaini muswada huu, aurejeshe
bungeni ufanyiwe marekebisho yenye kujenga kuaminiana na mwafaka wa
kitaifa kwenye mchakato wa mabadiliko ya Katiba. Hatutakwenda kumwona
ila aurejeshe bungeni,”alisema Lipumba na kuongeza:
“Mchakato huu unahitaji uvumilivu, staha na hekima
na usitawaliwe na nia mbaya, ubabe, mabavu, kejeli na dharau hasa
kutoka kwa watawala. Misingi hii ikipuuzwa mchakato mzima unaweza
kutumbukiza taifa letu katika mpasuko, migogoro na hata machafuko.”
Mwenyekiti huyo wa CUF alisema nchi ni mali ya
watu, hivyo mchakato huo haupaswi kuhodhiwa na chama kimoja, badala
yake unapaswa kuwa shirikishi na jumuishi ili kuwezesha kuandikwa kwa
Katiba katika msingi wa maridhiano.
Kuna madai kwamba muswada ulipitishwa ukiwa na
marekebisho ambayo yalifanyika kinyume na maoni ya wadau na kinyume hata
na makubaliano ya awali ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala
kuhusu mamlaka ya Rais kuteua wajumbe Bunge Maalumu la Katiba.
Madai mengine ni kwamba wabunge wa CCM waliongeza
baadhi ya mambo kupitia majedwali ya marekebisho, hivyo kutoa mwanya kwa
Serikali inayoongozwa na chama hicho kupitia kwa Rais kuwa na mamlaka
zaidi ya uteuzi wa wajumbe husika.
Itakumbukwa kuwa Septemba 6 mwaka huu, wabunge wa
CCM walitumia wingi wao kupitisha muswada huo katika mkutano wa Bunge
ambao ulisababisha tafrani kiasi cha Mbowe na Mbunge wa Mbeya Mjini,
Joseph Mbilinyi kutolewa nje ya Bunge kwa amri ya Naibu Spika, Job
Ndugai.
Katika tafrani hiyo, baadhi ya wabunge wa upinzani
walirushiana makonde na maofisa usalama, huku wabunge wote wa upinzani,
isipokuwa Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema, wakiususia.
Chanzo kutoka gazeti la mwananchi.
Chanzo kutoka gazeti la mwananchi.
Post a Comment