SHAHIDI wa tatu katika kesi ya matumizi
mabaya ya madaraka katika ujenzi wa jengo la ghorofa 18, lililo karibu
na Ikulu, Saimon Maembe ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa
Manispaa ya Ilala iliwanyima kibali washtakiwa katika kesi hiyo cha
kuongeza idadi ya ghorofa kwenye juu.
Kesi hiyo inawakabili vigogo wawili wa Wakala wa Majengo (TBA) ambao ni
aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa TBA, Makumba Togolai Kimweri na
Msanifu Mkuu wa TBA, Richard John Maliyaga.
Washtakiwa hao wanadaiwa kutumia madaraka yao vibaya kwa kutoa kibali
cha kupanua jengo hilo kwa kuongeza ghorofa tatu zaidi kutoka 15 hadi
18, bila idhini ya mamlaka husika na bila kufuata Sheria za mipango
miji.
Jengo hilo linalomilikiwa kwa ubia kati ya kampuni ya Royalle Orchard
Inn na TBA, liko katikati ya Jiji la Dar es Salaam, katika mtaaa wa
Chimara, kitalu namba 45 na 46, karibu na Taasisi ya Saratani Ocean
Road, katika Manispaa ya Ilala.
Akitoa ushahidi wake jana Mchunguzi wa kesi hiyo toka Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), alidai wakati anafanya
uchunguzi wake aligundua kuwa Manispaa ya Ilala ilikataa maombi ya
washtakiwa hao kujenga ghorofa 15.
Maembe alidai licha ya kuwa Wizara ya Ujenzi kutoa waraka kwa TBA
ikielekeza kuwa ni lazima ishirikishwe katika mchakato wa uendelezaji wa
viwanja vinavyomilikiwa na TBA kwa niaba ya Serikali, hata hivyo
washtakiwa hao hawakuishirikisha wizara hiyo katika mradi huo.
Maembe aliyekuwa akiongozwa na Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Leonard
Swai, kutoa ushahidi wake alieleza kuwa alianza kufanya uchunguzi wa
ujenzi wa jengo hilo baada ya Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu
Mizengo Pinda kutoa maelekezo kwa Takukuru, na kwamba alikabidhiwa
jukumu hilo na Kaimu Mkurugenzi wa Takukuru.
Alidai wakati akifanya uchunguzi wake alikwenda TBA ambako alipata
nyaraka mbalimbali za mradi huo kama vile tangazo la zabuni ya ubia wa
ujenzi wa jengo hilo, maombi ya wazabuni na taarifa ya tathmini ya
zabuni hiyo.
Alizitaja nyaraka nyingine kuwa ni mihtasari ya vikao na uamuzi wa Bodi
ya Zabuni ya TBA, mkataba wa ujenzi wa jengo hilo na vibali vya ujenzi,
na kwamba kampuni ya Royalle Orchard Inn ndio ilishinda zabuni hiyo na
kwamba nilibaini kuwa vibali vya ujenzi vilitolewa na TBA, jambo ambalo
lilimshangaza nikuona kuwa vibali vya ujenzi vilitolewa na TBA
wenyewe, kwa sababu haikuwa kawaida kwani kuna mamlaka zinazohusika na
vibali vya ujenzi.
Maembe alidai kuwa katika makubaliano ya ubia kati ya TBA na kampuni
hiyo, walikuabaliana kujenga jengo kwa ajili ya makazi na biashara na
kwamba jengo litakuwa ni la ghorofa 15.
Alidai kuwa kibali cha kwanza kilikuwa ni cha ujenzi wa ghorofa 15 na
cha pili kikiwa ni cha upanuzi wa mradi kutoka ghorofa 15 hadi 18 na
kwamba vyote vilitolewa na kusainiwa na mshtakiwa wa pili, Maliyaga.
Shahidi huyo alidai kuwa baadaye alikwenda Manispaa ya Ilala ambayo kwa
mujibu wa Sheria namba 8 ya Mipango Miji ya mwaka 2007 ndio yenye
mamlaka ya kutoa vibali, ili kuona kama walihusika kutoa vibali vya
ujenzi huo.
“Kiongozi wa Idara ya Mipango Miji alieleza kuwa waliwahi (washtakiwa)
kupeleka maombi ya kibali cha kujenga ghorofa 15 lakini wakayakataa,
kwa sababu hayakuendena na ramani ya mchoro wa eneo husika.”
Maembe alidai baadaye alikwenda Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi ambayo ndio yenye uamuzi wa mwisho ya matumizi ya ardhi, na
kwamba katika Idara ya Mipango Miji alipata ramani ya eneo husika ya
mwaka 2000.
Post a Comment