Mji wa Iringa uligeuka kuwa uwanja wa vita kati ya polisi wa
Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) na wafanyabiashara jana asubuhi. Watu
50 walikamatwa kutokana na tukio hilo akiwamo Mbunge wa Iringa Mjini
(Chadema), Mchungaji Peter Msigwa.
Katika vurugu hizo, gari la zimamoto lilivunjwa kioo na gari lingine dogo liliharibiwa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael
Kamhanda alisema Mchungaji Msigwa alikamatwa saa saba mchana kwa tuhuma
za kuhusika na vurugu hizo na kwamba watu wapatao 50 walikuwa
wamekamatwa katika fujo hizo zilizochukua karibu saa tatu.
“Mchungaji Msigwa amekamatwa kwa makosa ya
uchochezi, kufanya maandamano bila kibali na kuhamasisha watu kufanya
biashara kwenye eneo ambalo limekatazwa kisheria.
Tumemkamata na hatutamwachia hadi uchunguzi wa suala hili utakapokamilika. Pia na hao watu wengine,” alisema Kamanda Kamhanda.
Alisema waliamua kufanya doria katika eneo hilo
baada ya kupata taarifa za kiitelijensia kuwa wafanyabiashara walikuwa
na mpango wa kuwashambulia mgambo wa Iringa kama wangekwenda kuwazuia.
Post a Comment