Matokeo ya awali ya uchaguzi mkuu nchini Kenya yanaonyesha kuwa
Uhuru Kenyatta, mtoto wa Rais wa Kwanza wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta
anaongoza, huku akifuatiwa kwa karibu na aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi
hiyo, Raila Odinga.Kama alivyo Uhuru, Raila pia ni mtoto wa mmoja wa
waasisi wa taifa la Kenya, ambaye alikuwa Makamu wa Mzee Kenyatta,
Jaramong Oginga Odinga.
Hadi majira haya ya saa 6.45 usiku wa kuamkia
leo, Uhuru ambaye ni mgombea wa TNA alikuwa amepata kura 744,648 sawa
na asilimia 56.1 wakati Raila ambaye ni mgombea wa ODM alikuwa akifuatia
kwa kupata kura 527, 780 sawa na asilimia 39.7.Matokeo hayo ni kutoka katika vituo zaidi ya 5000
kati ya 31,000 na yalikuwa yakionyeshwa moja kwa moja na Tume Huru ya
Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) kadri yalivyokuwa yanaingia.
Hata hivyo Mwenyekiti wa IEBC, Isaack Hassan
akizungumza na vyombo vya habari jana usiku alisema matokeo hayo ni ya
awali na kwamba matokeo kamili yangetangazwa na tume yake baada ya
kukusanya taarifa kutoka vituo vyote vya kupigia kura.
Wagombea wengine walikuwa wameachwa mbali. Hao ni
Musalia Mudavadi, Peter Kenneth, James Kiyiapi, Martha Karua, Mohamed
Dida na Paul Muite.
Chanzo Gazeti Mwananchi





Post a Comment