Social Icons

Loading...

Mimi siyo Rais, asema Lowassa .

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowasa amewataka waendesha bodaboda na watu wengine wasimwite Rais kwa sababu wanamtengenezea chuki na uhusiano mbaya na watu.

“Mbona mnataka kuniletea uchuro! Mnanitengenezea ugomvi na watu jamani…,” alisema wakati akizindua Shirikisho la Bodaboda Tanzania jana kwenye Viwanja vya Leaders, Dar es Salaam.

Lowassa amekuwa akitajwa kuwania urais katika uchaguzi ujao wa Rais na wabunge utakofanyika 2015. Hatua hiyo imekuja baada ya Lowassa kuwaeleza kuwa atafanya harambee ya kuchangisha fedha ili kila aliyeingia kwenye shirikisho la waendesha bodaboda aweze kupata pikipiki yake.

Baada ya kauli hiyo waendesha bodaboda hao walipaza sauti zao wakiimba rais,rais …..wa mwaka 2015 huku wakidai amepita hana mshindani. Aliwataka kuacha  kumwita rais kwa sababu wanamtengenezea ugomvi na watu.

Alisema asilimia 50 ya madereva wanaoendesha  bodaboda hizo siyo pikipiki zao hivyo kutokana na hilo atafanya harambee ili kila mmoja kumiliki  pikipiki yake ili waweze kujiajiri wenyewe.

“Tumeona kuna tofauti kubwa kati ya matajiri na maskini hivyo nimeona kwenye shirikisho hili asilimia 50 siyo za kwenu.  Nimekusudia kuanzisha  harambee ya madereva ambao hawana pikipiki ili nao  wawe nazo waweze kujiajiri,” alisema Lowasa.

Lowasa aliitaka Kamati ya Shirikisho la Bodaboda kukutana naye Januari 15 mwaka 2014 ili kupanga harambee hiyo ifanyike lini na wapi.

Alisema matajiri nchini wapo wengi nitawafuata na kuwachangisha harambee wakiwemo Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi na mfanyabiashara maarufu Said Salum Bakhresa.

SIMBA YAIBAMIZA YANGA 3 -1 , YATWAA KIKOMBE CHA MTANI JEMBE.

Mshambuliaji Amis Tambwe ameitibua sherehe ya utambulisho wa Emmanuel Okwi baada ya kupachika  mabao mawili wakati Simba ilipoichakaza Yanga 3-1 katika mchezo wa ‘Nani Mtani Jembe’ jana kwenye Uwanja Taifa, Dar es Salaam.
Mrundi Tambwe  alifunga mabao mawili huku Awadh Juma akifunga bao moja kwa Simba kabla ya Okwi kufunga bao la kufutia machozi kwa Yanga.
Tambwe aliwainua mashabiki wa Simba dakika ya 13 baada ya kupokea pasi nzuri ya Said Ndemla akiwa peke yake na kupiga shuti pembeni kwa kipa Juma Kaseja.
Baada ya Simba kupata bao mashabiki wa Yanga walikaa kimya hali iliyomfanya mwenyekiti wao Yusuf Manji kusimama na kuwataka washangilie huku akionyesha vidole vitano. Jambo lililowafanya mashabiki wa Simba kuanza kuzomea kwa nguvu.
Tambwe alipatia Simba bao la pili kwa mkwaju wa penalti dakika ya 43 baada ya Ramadhani Singano kuchezewa vibaya na David Luhende, kabla ya kuhitimisha kwa bao la tatu dakika ya 60, akitumia vizuri uzembe wa Kaseja kupachika bao la tatu.
Manji aliinuka kwenye kiti chake na kwenda kumkumbatia Zaccaria Hanspope na kuondoka uwanjani hali iliyowafanya mashabiki wa Simba kumzomea.
Okwi aliingia akitokea benchi na kuifungia Yanga bao la kufutia machozi dakika ya 79, akimalizia vizuri krosi ya Haruna Niyonzima.
Mashabiki wa Simba walikuwa wakiwakejeli wenzao wa Yanga kwa kuwaambia waendelee kusajili wachezaji wa Simba faida yake wameiona.
Baada ya kukabidhiwa kombe mashabiki wa Simba walizunguka nalo, na wengine wakisukuma gari la Hanspope huku wakiimba ‘Okwi, Okwi, Okwi..’
Katika mchezo huo Yanga walionekana kuwa na presha na kucheza zaidi kibinafsi kuliko kitimu kulinganisha na wapinzani wao Simba.
Yanga waliondoka kabisa mchezoni baada ya bao la Simba na kuwaacha viungo Mkude, Henry Joseph, Chombo wakifanya watakalo katika kuanzisha mashambulizi ya vijana hao wa Msimbazi.

KIBONZO


Mandela AIVUTA DUNIA S.A.



Viongozi zaidi ya sabini wakiwamo wakuu wa nchi na Serikali wanatarajiwa kushiriki hatua mbalimbali za safari ya mwisho ya Mzee Mandela aliyefariki Alhamisi ya Desemba tano usiku.

Anatarajiwa kuzikwa Jumapili ijayo, Desemba 15, 2013 katika Kijiji cha Qunu alikokulia, mazishi ambayo yanatarajiwa kuwavuta maelfu ya watu kutoka kona mbalimbali za dunia.
Hata hivyo hadi jana maofisa wa Serikali ya Afrika Kusini walisema walikuwa bado hawajapata orodha kamili ya viongozi wote watakaohudhuria, l pia wakashindwa kusema iwapo Rais Obama atakwenda Qunu au atashiriki katika hatua nyingine za awali za msiba huo kabla ya mazishi ya Jumapili.
Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Jay Carney alinukuliwa akithibitisha kwamba Obama na mkewe Michele watashiriki katika msiba huo lakini hakuwa tayari kueleza suala hilo kwa undani. Habari zaidi zilizopatikana jana mjini Johanesburg zinasema Rais wa Brazil, Dilma Rousseff atakuwa miongoni mwa wageni mashuhuri watakaoshiriki.
Balozi wa Marekani nchini Afrika Kusini, anasema kuwa: “Rais Obama, amethibitisha kushiriki mazishi ya Madiba” (akirejea) jina maarufu la Mzee Mandela, taarifa ambayo ilitiliwa na nguvu na habari zilizoinukuu Ikulu ya Washington ikithibitisha ujio wa kiongozi huyo pamoja na watanguliza wake; George W. Bush na Bill Clinton.

Azimio la kuwataka Ghasia, Mwanri na Majaliwa kujipima lapitishwa.

Bunge limepitisha azimio la kuwataka mawaziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kujipima iwapo wanatosha kuendelea kuongoza wizara hiyo nyeti.
Azimio hilo lilipitishwa jana na wabunge kwa kura ya ndiyo bila kupingwa, baada ya kuhojiwa na Spika wa Bunge Anne Makinda iwapo wanaipokea taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (Laac) iliyowasilishwa na Mwenyekiti wake Rajabu Mbaruku.
Moja ya mapendekezo yake ni Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia na manaibu wake, Aggrey Mwanri na Kassim Majaliwa kujipima kama wanatosha kuendelea kuongoza wizara hiyo kutokana na kugubikwa na vitendo vya ufisadi.
Kwa mujibu wa taratibu za Bunge, taarifa ya kamati inapowasilishwa na kupitishwa pamoja na mapendekezo yake, huwa ni azimio kamili ambapo Serikali hutakiwa kutoa maelezo ya utekelezaji wake.
Kabla ya azimio hilo kupitishwa, Mwenyekiti wa Laac, Rajabu Mbaruku alijibu michango ya wabunge waliochangia katika taarifa ya kamati yake iliyowasilishwa Ijumaa iliyopita, akiwemo Waziri Ghasia.
Akizungumza baadaye, Mbaruku alisema hayo ndiyo mapendekezo na Serikali itatakiwa kuyatolea maelezo ya jinsi yatakavyotekelezwa. “Hata waziri mkuu nimemtaja kwa jina, na nimesisitiza kama ananisikia kuhusu ofisi yake,” alisema.
Katika mchango wake, Waziri Ghasia alijaribu kupangua tuhuma mbalimbali zilizoelekezwa katika wizara yake ikiwamo kuwapo ufisadi, ubadhirifu na mtandao wa wizi unaohusisha Hazina, Wizara na Halmashauri.
Ghasia alikiri Halmashauri ya Mbarali ilitumiwa fedha kuliko kiwango kilichoidhinishwa na Bunge na kwamba
suala la halmashauri mbili za Tanga kupewa zaidi ya Sh2 bilioni haikuwa sahihi bali yalikuwa ni makosa ya Mkaguzi Mkuu wa Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG).
Kuhusu ufisadi wa zaidi ya Sh600 milioni zilizotolewa na wafadhili kwa ajili ya mpango wa maboresho ya Serikali za Mitaa, alisema haamini kama maneno yaliyonukuliwa na vyombo vya habari kuhusu fedha hizo yalisemwa na wafadhili.
Wafadhili wa mradi huo walinukuliwa wakilalamikia ufisadi huo na kudai kwa sasa hawana la kufanya na wanamwachia Rais, huku wakieleza kushangazwa na Rais kuteua watu dhaifu kuendesha
© Copyright Daniel Blog in Contemporary News
Back To Top